Olympique Lyon inapamba kujinusuru kushushwa daraja mwisho wa msimu kutokana na masuala ya kiuchumi yanayoikabili na imepanga kuwauza mastaa wake ili kupata pesa za kujiimarisha.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi uliofanywa na taasisi ya kufanya uchunguzi wa kiuchumi katika soka nchini humo kubaini klabu hiyo inakabiliwa na madeni yaliyopitiliza kutokana na matumizi yanayozidi kipato ambacho timu hiyo inaingiza.
Mwandishi wa habari za michezo nchini Ufaransa, Romain Molina amefichua Lyon imewaweka sokoni wachezaji wake wote kama njia mojawapo ya kupunguza deni ambalo linaikabili.
Suala la kuwekwa sokoni hapana shaka ni habari mbaya kwa nyota mbalimbali wakiwemo waliowahi kucheza katika Ligi Kuu England.
Miongoni mwa nyota wanaoichezea Lyon ni Wilfried Zaha, Alexandre Lacazette, Nemanja Matic, Said Benrahma, Ainsley Maitland-Niles, and Jordan Veretout. Pia wapo kina Anthony Lopes, Corentin Tolisso, Rayan Cherki, Gift Orban na Georges Mikautadze.
Lyon imekuwa na matumizi makubwa ya fedha mwaka hadi mwaka na mfumo wake wa kifedha umekuwa ukitegemea mwendelezo wa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kutangaza madeni yenye thamani ya Pauni 422 milioni, timu hiyo imepewa adhabu ya kutosajili wachezaji na kwa mujibu wa vyombo vya habari Ufaransa, mwishoni mwa msimu itashuka daraja ikiwa hali yake ya kiuchumi haitatengamaa.
Georges Mikataudze
Ikiwa hilo litatokea Lyon itafuata nyayo za Bordeaux ambayo ilishushwa hadi Ligi Daraja la Tatu Ufaransa baada ya kufilisika.
Mmiliki mwenye asilimia nyingi ya hisa za Lyon, John Textor ambaye pia ni mmiliki mwenza wa Crystal Palace inayoshiriki Ligi Kuu England alisema licha ya juhudi kubwa ambayo amefanya kuishawishi serikali ya Ufaransa isichukue uamuzi huo, hakuna kilichobadilika.
Hata hivyo, timu hiyo haijashiriki mashindano yoyote makubwa Ulaya tangu msimu wa 2019/2020 ilipofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.