Kocha wa Liverpool Arne Slot ameanza vizuri msimu huu akishinda mechi 15 kati ya 17 akipoteza mchezo mmoja na sare moja, huku wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, majogoo hao wa Jiji la Liverpool watakuwa na siku 18 ngumu kuanzia jana.
Ugumu huo wa siku hizo unatokana na hali ya mikataba ya wachezaji wao tegemeo Mohamed Salah, Virgil van Dijk, na Trent Alexander-Arnold ambao wakishindwa kufikia makubaliano ya kuwasainisha mikataba mipya ndani ya siku hizo, hatari ya kuwakosa itakuwa ni kubwa.
Siku 48 ni hadi kufikia Desemba 31, ambapo baada ya hapo dirisha la majira ya baridi litafunguliwa rasmi nchini England na mastaa wote hao watakuwa na nafasi ya kuzungumza na timu ya nje ya England pia watakuwa na uwezo wa kusaini mkataba wa awali.
Licha ya taarifa za uwezekano wa kuondoka kwao kuanza kusambaa kabla ya kuanza kwa msimu huu, Liverpool ilidaiwa kufanya mazungumzo na wawakilishi wao lakini hawakufikia mwafaka.
Wakala wa Salah, Ramy Abbas Issa, mara kadhaa amewahi kujibu mara nyingi maswali ya hatma ya staa huyo wa Misri na alikuwa akisema bado hakuna kilichoamuliwa.
Salah yuko kwenye kiwango kizuri sana na yeye ndiye mchezaji wa kwanza katika ligi tano kubwa za Ulaya kufikisha magoli 10 na asisti 10 msimu huu na ikiwa ataondoka Liverpool huenda ikatumia walau Pauni 100 milioni kutafuta mbadala wake.
Ripoti zinaeleza Liverpool inataka kusikilizia hadi siku hizo 48 zitakapoisha na ikiwa mastaa hao wote watagoma kusaini mkataba mpya basi wanaweza kuwauza ili kuepuka hasara ya kushuhudia wakiondoka bure mwisho wa msimu.
Hadi sasa hakuna dalili ya kufikia makubaliano ingawa mabosi wa Liverpool wanafanya kazi ya ziada kufanikisha hilo na moja ya changamoto zinazotajwa ni kiasi cha pesa ambacho wachezaji hawa wanakihitaji ili kusaini mkataba mpya.
Salah ambaye anakunja Pauni 350,000 kwa wiki anataka karibia 450,000 ili kubaki wakati Trent anayewindwa na Madrid anataka kupewa mshahara mkubwa zaidi kuliko mchezaji yoyote sawa na ilivyo kwa Van Dijk anayehitaji mshahara unaokaribia na Salah.