TAARIFA njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba baada ya kumalizana na, Ladack Chasambi wa Mtibwa Sugar, mabosi wa timu hiyo tayari wamekamilisha dili jingine la jembe la kwanza la kimataifa ambalo linatarajiwa kutua ndani ya timu hiyo kupitia dirisha dogo la usajili.
Spoti Xtra, tayari limepata taarifa za mapema juu ya Simba kukamilisha usajili wa kwanza wa kimataifa kwa kumshusha kiungo mkabaji anayeitwa, Mika Miche mwenye umri wa miaka 27 ambaye ni raia wa DR Congo.
Kiungo huyo ambaye amewahi kutamba katika kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo na klabu ya TP Mazembe kwa sasa anakipiga katika klabu ya FC Lupopo.
Chanzo chetu makini kutoka DR Congo kimelipa taarifa za ukweli Spoti Xtra, juu ya Simba kukamilisha usajili wa kiungo huyo mkabaji kutokana na kocha Benchikha kuhitaji ongezeko la mchezaji katika nafasi hiyo kupitia dirisha dogo la usajili.
“Mika Miche anatarajiwa kujiunga na Simba ambao waliambiwa watafute kiungo mkabaji na kocha Benchikha, mchezji huyo atajiunga na Simba dirisha dogo kama kila kitu kitakuwa sawa, mkataba wake na FC Lupopo upo ukingoni, hivyo Simba wamekamilisha kila kitu kutoka kwa upande wa mchezaji kwa kuwa upande wa timu hauna uwezo wa kumzuia kwa kuwa mkataba wake upo ukingoni,” kilisema Chanzo hiko.
Hata hivyo pia Spoti Xtra, halikuishia hapo ndipo lilipomtafuta meneja wa mchezaji huyo anayefahamika kwa jina la, Faustino Mukandila ambaye yeye alisema kuwa: “Ni kweli Mika Miche mwezi Januari kwa maana ya dirisha dogo nina uhakika atajiunga moja ya timu kubwa kutoka Tanzania.
“Siwezi kusema ni timu gani kwa kuwa ni makubaliano ya siri ya pande zote mbili kwahiyo kama kila kitu kitakuwa sawa basi watu watafahamu juu ya dili hili,”alisema meneja huyo wa Mika miche kutoka katika kampuni ya Soccer Bro Manegement inayomiliki wachezaji wengi barani Afrika.