CR7 KAUKATAA UKOCHA

Cristiano Ronaldo amesema kinachomfanya aendelee kucheza kwa sasa ni motisha na pindi atakapostaafu hana mpango wa kugeukia ukocha.


Ronaldo ambaye hivi karibuni atafikisha miaka 40, alifunga mabao mawili katika ushindi wa 5-1 ilioupata Ureno dhidi ya Poland kwenye mchezo wa Uefa Nations League uliopigwa juzi.


Kutokana na mabao hayo mchezaji huyo anaendelea kuisogelea rekodi ya mabao 1000 ambayo anadai ndio inayosababisha aendelee kupambana hadi sasa. Kwa sasa ana mabao 909 aliyofunga katika maisha yake ya soka.


Wakati akionekana anaelekea ukingoni, Ronaldo ameonyesha hajapanga kustaafu soka hivi karibuni na wala hafikirii hilo kwa sasa.


Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Poland alisema atakapoamua kuachana na klabu na timu ya taifa atafanya hivyo, lakini kwa umakini zaidi.


"Sijioni nikisimamia timu (kama kocha). Hiyo siyo katika mipango yangu. Baada ya soka nitajiendeleza katika maeneo mengine ingawa muda utasema nini kitafanyika," alisema.


Ronaldo kwa sasa amebadilisha mtindo wake wa uchezaji akicheza zaidi kama mshambuliaji wa kati badala ya winga alivyokuwa akicheza awali.


Mara kadhaa awali alipoulizwa kuhusu hatima yake alikataa kuonyesha kwamba atastaafu hivi karibuni akisisitiza kuwa na malengo mengi mbeleni.


"Nataka tu kufurahi.Suala la kupanga kustaafu sijui kama litatokea katika mwaka mmoja au miwili. Nakaribia miaka 40 hivi, nataka kufurahi hadi nitakapojihisi siwezi nitastaafu." 


Pia alisema moja ya mambo ambayo yanasababisha asitamani kustaafu mapema ni kufikia ombi la mwanawe ambaye amtaka kusubiri ili siku moja waweze kucheza pamoja uwanjani. 


"Mwanangu ananiambia 'baba, subiri miaka michache nataka kucheza na wewe," alisema mchezaji huyo mwaka juzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post