Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeanzisha uchunguzi kuhusu vurugu zilizotokea baada ya mchezo kati ya Morocco dhidi ya DR Congo.
CAF inazichunguza Shirikisho la Soka Morocco FRMF na lile la Congo FECOFA kutokana na tukio hilo la baada ya mchezo ambalo maofisa wa timu ya Morocco na DR Congo walikunjana na kusukumana katika vurugu hizo na zilianza kwa kocha wa Morocco na Walid Regragui na beki wa DR Congo, Chancel Mbemba.
Video zilionyesha watu kutoka kambi zote mbili wakitoleana maneno na kusukumana baada ya mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 1-1 huku majibizano ya awali yakianzia kwa Regragui na Mbemba.
Wachezaji na maofisa walirekodiwa wakikimbilia kwenye vyumba vya kuvalia, huku aliyerekodi video hiyo akidai polisi zaidi waliitwa uwanjani hapo.
Mwandishi wa habari mmoja aliyerekodi video hiyo alidai Regragui alimfuata Mbemba wakati beki huyo akiwa amepiga magoti akisali na kusababisha wawili hao kujibizana.