Watu wawili wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamefariki Dunia na wengine ambao idadi kamili bado haijafahamika kujeruhiwa baada ya kutokea Mlipuko uliosababisha Moto kwenye Moja ya Ghala lililokuwa na wafanyakazi wakiendelea na majukumu yao.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Kamishna msaidizi wa Polisi Alex Mukama akizungumza kwa njia ya Simu amesema Mlipuko huo ambao chanzo chake hakijafahamika, ulitokea April 12 na baada ya kupata taarifa alifika eneo la tukio na kuungana na wataalam wengine kufanya uchunguzi, lakini tayari watu wawili walikwisha fariki pia wapo waliojeruhiwa.
Miili ya watu hao wawili ilipokelewa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro usiku huo wa April 12, ambapo kwa mujibu wa Kaimu Afisa Mahusiano wa Hospitali hiyo Scholastica Ndunga walio fariki wamekwisha tambuliwa kwa majina ambao ni Hamis Said (29) na Frenk Kennedy (26).
Tangu taarifa za kutokea Mlipuko huo ambao umesababisha Moto uliozua maafa, baadhi ya watu Kujeruhiwa pia kuteketeza sehemu ya Ghala la Kiwanda huko eneo la Loliondo Dakawa, hakuna taarifa zaidi za ufafanuzi juu ya undani wa Tukio lenyewe, ukiachana na taarifa za hospitali ya Rufaa ilipohifadhiwa miili ya waliofariki.
Aidha bado jitihada zinaendelea kufuatilia kwa viongozi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, pia viongozi wengine wenye mamlaka ikiwemo Jeshi la Polisi na viongozi wengine wa serikali, kujua undani wa tukio lenyewe, ikiwemo chanzo cha Mlipuko pia madhara yaliyo jitokeza.
Tags
#KITAIFA