Afisa Habari wa Klabu hiyo, Thabit Zacharia Zaka’ amesema kuwa, timu kubwa kama Azam FC itakuwa ni stori kubwa kwenye vyombo vya habari kama Dirisha Dogo litapita bila kufanya usajili.
Pamoja na hayo yote amesema jukumu lote wanamuachia Kocha wao Mkuu, Youssouph Dabo, ambaye ndiye atakuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mchezaji anayemtaka.
“Usajili ni muhimu, timu kubwa kusajili ndiyo maisha yake ndiyo chakula chake, isiposajili ndiyo inakuja stori kwamba timu fulani haijasajili, kama hatutosajili ni lazima tutatengeneza habari kubwa kwenye vyombo vya habari, ila naweza kusema tu tutafanya usajili kuboresha sehemu chache, kuna sehemu zinahitaji kuongeza watu kwa sababu wengine wanaumia hivyo mapungufu lazima yataonekana, kwa hiyo lazima tutafanya usajili wa maboresho,” amesema Zaka.
Aidha, amesema msimu huu wanauhitaji ubingwa kwa udi na uvumba na mpaka sasa wapo nafasi ya pili kwa pointi 19, hivyo wataongeza wachezaji kwa ajili ya kuwasaidia waliopo.
“Najua yote haya inategemea pia matakwa ya kocha, anaweza akasema hawa wanatosha, lakini tunamuachia yeye maamuzi yote, kama akiangalia akaona kuna umuhimu kuongeza nguvu kazini tutafanya hivyo kwa sababu tayari tumetenga bajeti ya usajili, akisema anataka kuongeza mtu au watu atasaidiwa tu kwa sababu klabu tayari ina bajeti ya usajili.” amesema Zaka.
Amesema timu yao bado ipo kwenye mbio za ubingwa na kwamba kuna michezo mingi ya Ligi Kuu mbele yao hivyo kama watachanga karata zao vizuri kwenye michezo hiyo nafasi ya ubingwa bado wanayo.