Mvua Kubwa Iliyoambatana na kimbunga imebomoa mapaa ya Zaidi ya Nyumba 30 Kijiji cha Nebuye kata ya Ngoma wilaya ya Ukerewe mkoa wa Mwanza.
Kimbunga hicho kiliibuka majira ya saa tano asubuhi tarehe 29.11.2022 wakati mvua ikinyesha katika maeneo mbalimbali wilayani hapo na kuathiri makazi ya watu, kanisa, ofisi za serikali na chama CCM na kuezua vyumba vya madarasa katika Kijiji cha Nebuye chenye kitongoji cha Mwitawi, Shuleni, Hamurumo, Kati, Nabuta, Ofisini na Kongola.
Kitongoji cha Mwitawi ndicho kilichoathirika zaidi kwa kuezuliwa zaidi ya nyuma (makazi ya watu) 20, nyumba nyingine zilizoezuliwa zinatoka katika vitongoji vya Shuleni, Hamurumo, Kati, Nabuta, Ofisini na Kongola ambapo zaidi ya nyumba 30 katika Kijiji hicho zimeezuliwa.
Vilevile madhara yametokea Kwenye kanisa la Anglikana, Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi CCM tawi, Shule ya Msingi Butiriti imeezuliwa ofisi ya walimu na vyumba vitatu vya madarasa na kuathiri Mali zilizokuwemo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Col. Denis Mwila amefika eneo hilo mapema leo akiambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya.
Wengine waliofika ni Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Mang'oha Maginga na viongozi wa eneo hilo kwa lengo la kuwapa pole na kupata uhalisia wa tukio Hilo.