Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya Sekta ya Ufugaji nyuki hapa nchini kwa kuhakikisha asali yote inayozalishwa inakuwa na ubora na viwango vinavyotakiwa ili iweze kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka alipokua akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Ufugaji Nyuki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema kupatikana kwa soko la uhakika la asali kutawawezesha wananchi hususani wanaojishughulisha na ufugaji nyuki kuongeza uzalishaji wa asali kutokana kuwa na uhakika wa soko la asali na bidhaa zitokanazo na mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki hivyo kuongeza Pato la Taifa.
" Kati ya mikakati ambayo tumeifanya ni pamoja na kuwasiliana na Serikali ya China na wameshakubali kuchukua asali yetu kwa kuzingatia kiwango ambacho Tanzania tumetengewa, kazi iliyobaki sasa ni kujua kiasi gani tutapeleka kwa kuwa Serikali ya China inapofanya kazi huwa inatenga kota ya kiwango cha asali cha kuingiza kwa mwaka" Ameeleza Prof. Sedoyeka.
Aidha, amebainisha kuwa miaka michache iliyopita kulikuwa na kampuni ya China iliyokuwa wilayani Kibaha mkoani Pwani ambayo ilikuwa ikichukua asali hapa nchini na kuipeleka China, hata hivyo ilifunga biashara yake kutokana na mabadiliko ya kiuchumi duniani.
" Kufungwa kwa kampuni hiyo hiyo kuliyumbisha kidogo uhakika wa soko la asali nchini China, hata hivyo tumeshafanya juhudi mbalimbali kulishughulikia jambo hili, Pia tunao wafanyabiashara wetu wanaopeleka asali ya Tanzania nchini Marekani na Ulaya ambako wameonesha wana mahitaji ya asali yetu " Amesisitiza Prof. Sedoyeka.
Ameongeza kuwa Tanzania ina faida ya kuwa na maeneo mengi yanayozalisha asali jambo ambalo linaiongezea sifa asali ya Tanzania kuwa ya aina tofauti tofauti jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani kwenye soko la dunia kutokana na ubora wa asali inayoyazalishwa hapa nchini.
" Sisi tunauhakika kwamba tukiendeleza jitihada hizi tutafika mahali ambapo asali ya Tanzania itakuwa ni moja kati ya bidhaa tunazo uza nje na kuingizia fedha za kigeni"