AUAWA KISA MIHOGO



Mkazi wa kitongoji cha Ikoni B, kata ya Buzilasoga, Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Getruda Dotto amepoteza maisha baada ya kundi la watu kufika nyumbani kwake likiongozwa na Diwani wa Buzilasoga, Daudi Shilinde na Emmanuel Makala, Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Ikoni B na William Nengo ambaye ni Kamanda wa Sungusungu na Mwenyekiti wa CCM kijiji cha Ikoni B.

Viongozi hao pamoja na kundi hilo la watu walikuwa wakimtuhumu Getruda Dotto kwa kosa la wizi wa mihogo toka kwenye shamaba la Scolastika John.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewaeleza waandishi wa habari kuwa, awali shamba hilo liliuzwa na wanaukoo siku ya msiba wa Ndebete Mzee Miharalo ambaye alikuwa mume wa Getruda Dotto.

Kamanda Mutafungwa amesema, pamoja na mwanamke huyo kujitetea kuwa shamba alilochimba mihogo ni mali ya marehemu mume wake watu hao wenye hasira kali pamoja na viongozi wao waliendelea kumshambulia kwa kutumia fimbo na rungu na hatimaye walikusanya majani na vipande vya miti kisha kumchoma moto na kusababisha kifo chake.

Pia wahalifu hao walichoma nguo pamoja na kubomoa nyumba aliyokuwa akiishi marehemu na Watoto wake wawili wa kike.

Kamanda Mutafungwa amesema kuwa baada ya uchunguzo wa polisi imegundulika kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi uliojitokeza 
baada ya mume wa marehemu aitwaye Ndetebe Mzee Miharalo kufariki na kuacha shamba hilo la mihogo ambalo wanaukoo waliliuza bila kumshirikisha mke wa marehemu ambaye ni Getruda Dotto.

Post a Comment

Previous Post Next Post