DAR ES SALAAM: Waziri wa utamaduni,Sanaa na michezo Dk,Damas Ndumbaro ameitakia kila la heri timu ya kikapu ya pazi na kuahidi kuiunga mkono timu hiyo inayokwenda Nchini Afrika kusini kushiriki mashindano ya hatua ya 16 bora ya kufuzu fainali za mpira wa kikapu Afrika
Dk.Ndumbaro amesema hayo leo Novemba 17,2023 jijini Dar es salaam wakati akiongea na waandishi wa habari katika hafla ya kuiaga timu hiyo
Aidha,Dk.Ndumbaro ameuomba ubalozi Tanzania Nchini Afrika kusini uipokee timu hiyo na kuwaomba watanzania walioko nchini humo wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo katika kipindi chote itakapokuwa kwenye mashindano hayo
“Tunaamini pazi itafanya vizuri, tunawasiliana na Balozi wa Afrika kusini ili awahamize watanzania wajitokeze kuwashangilia na kuwaunga mkono kipindi chote mtakachokuwa huko ili muweze kufanya vizuri”amesema Dk. Ndumbaro
Kwa upande wake Kocha wa timu ya Pazi Henry Mwinuka amesema timu itaondoka Alfajiri ya kesho kuelekea nchini humo.
Amesema mashindano hayo ni hatua ya 16 yataanza Novemba 21 hadi 26, Mwaka huu ambapo Tanzania ipo kundi A ikiwa na timu za Cape Town ya Afrika kusini,NBA Academy na Dynamos ya Zambia.
Washindi wa kundi hilo wataingia hatua ya nusu fainali na kukutana na timu mbili za kundi B kutafuta washindi watatu watakaoungana na timu tisa(9) zilizofuzu kwaajili fainali hizo.