WATUMISHI WAASWA KUITETEA SERIKALI


Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tumepewa dhamana ya kuitetea Serikali na taasisi zake kwenye mashauri ya madai na usuluhishi ndani na nje ya nchi Tanzania ili kulinda maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Nalija Luhende wakati akizungumza na menejimenti na wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kwa mara kwanza baada ya kuapishwa kutumikia cheo hicho na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa makabidhiano ya Ofisi hiyo na Naibu Wakili Mkuu Mkuu wa Serikali, Bi. Sara D. Mwaipopo aliyeteuliwa kushika wadhifa huo.

Dkt. Luhende amewataka watumishi hao kuendelea kupambana na kusimamia haki na sheria na kulinda mali za Serikali kama alivyosema Mhe. Rais Samia kuwa ni Mawakili ni mainjinia wa haki na tumepewa dhamana ya kuitetea Serikali na taasisi zake kwenye mashauri ya madai na usuluhishi ndani na nje ya Tanzania.

“Katika kipindi hiko ambacho Rais wetu Mhe. Samia anafanya jitihada kubwa sana katika kuvutia wawekezaji nchini, sisi kama Ofisi inayosimamia mashauri ya madai na usuluhishi yaliyofunguliwa dhidi au kwa niaba ya Serikali tuna jukumu la kuhakikisha kuwa haki inatendeka ili kudumisha imani kwa wawekezaji” amesema Dkt. Luhende.

Ameeleza kuwa kwa kusimamia haki kutasaidia kumaliza migogoro kwa wakati na kwa kufuata haki na sheria, kudumisha uhusiano kati ya Serikali na wawekezaji, kujenga imani kwa wawekezaji kuhusu hali ya utoaji haki ili kukuza diplomasia ya uchumi nchini.

Dkt. Luhenda amewata watumishi kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uwazi, uwajibikaji, uadilifu na weledi kwa maslahi mapana yaTaifa na kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano ili kuhakikisha wanaitetea Serikali kwa ufanisi na kuwa mstari wa mbele katika kujenga uchumi wa nchi.

Akimkaribisha Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Duncan Mwaipopo amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa kutambua kuwa wote wana wajibu wa kusimamia vema rasilimali watu na fedha kwa kuzingatia sheria, tararibu na kanuni za utumishi wa umma ili kuwa na utendaji wenye tija, kuleta matokeo makubwa na ufanisi kwa lengo la kuendelea kujenga taswira nzuri iliyopo kwa wadau wetu, wananchi na taifa kwa ujumla.

“Ni imani yangu kuwa kila mmoja wetu atasimama katika nafasi yake na kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia taaluma zetu, weledi, ujuzi, uzoefu na kulinda maslahi mapana ya taifa letu huku tukizingatia dhana ya uwazi, uwajibikaji, na kufanya kazi kama familia moja kwa kuwa tunatumia muda mwingi kuwa Ofisini tukitekeleza majukumu yetu hivyo ni muhimu kuendelea kudumisha umoja, upendo na mshikamano” amesema Bi. Mwaipopo
 
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya OWMS, ndugu George Mandepo, Mkurugenzi wa Usuluhishi wa OWMS amewapongeza viongozi hao kwa kuaminiwa na kuteuliwa na wajumbe wa Menejimenti wako tayari kuwapa ushirikiano, watapokea maelekezo na miongozo kutoka kwao ili kuendelea kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo
Naye Mary Akonaay, Mhasibu wa OWMS akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi hiyo, wanamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumteua Dkt. Luhende kuwa Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuwa katika uongozi wake akiwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali amewajali watumishi na kuwaweka pamoja hivyo watumishi walimpatia ushirikiano wa kutosha katika kazi zake na utendaji wa watumishi hao umefanyika daraja la kupandishwa cheo na pia wamemuhakikishia Bi. Mwaipopo ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake mapya

Akitoa taarifa kuhusu muundo na mjukumu ya OWMS, ndugu James Kibamba, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa OWMS amewaeleza viongozi hao kuwa tangu kuundwa kwa OWMS mwaka 2018; Ofisi hiyo ina Idara tano na Vitengo saba ambazo ni Idara ya Utumishi wa Utawala; Idara ya Mipango; Idara ya Usuluhishi; Idara ya Menejimenti ya Kesi na Udhibiti Ubora; Idara ya Madai; pamoja na Vitengo vifuatavyo ikiwemo Kitengo cha Fedha na Uhasibu; Manunuzi na Ugavi; TEHAMA; Masjala ya Sheria; Maktaba na Utafiti; Ukaguzi wa Ndani; na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambapo amewahakikishia viongozi hao kuwa Ofisi hiyo ina wataalam wa kada mbali mbali, wenye weledi, ujuzi na uzoefu hivyo wako tayari kushirikiana nao kufanikisha utekelezaji wa majukumu ambayo wamekasimiwa na Serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post